SHAIRI : NI NANI KAMA MWALIMU!? - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI : NI NANI KAMA MWALIMU!? (/showthread.php?tid=1972) |
SHAIRI : NI NANI KAMA MWALIMU!? - MwlMaeda - 01-03-2022 NI NANI KAMA MWALIMU!? ———————————— 1.Naja nikiwakumbusha kuipitia nudhumu, anayejenga maisha, laazizi maalimu, yule alotufundisha, kwanza kushika kalamu, NI NANI KAMA MWALIMU, HUSUSAN WA MSINGI? 2. Nalola siku ya kwanza, nikipelekwa shuleni, na wakati nilianza, kuingia darasani, mwalimu alinifunza, ‘lufabeti kwa makini, NI NANI KAMA MWALIMU, HUSUSAN WA MSINGI? 3. Sana nilizikariri, herufi alonifunda, tena nikiwa mahiri, wa nyimboze nilopenda, hadi leo ninakiri, nafaidi ye matunda, NI NANI KAMA MWALIMU, HUSUSAN WA MSINGI? 4. Nakumbuka nikianza, kuandika mchangani, kalamu yangu ya kwanza, ni kijiti wajameni, Huyo aliyenifunza, mgee kheri Manani, NI NANI KAMA MWALIMU, HUSUSAN WA MSINGI? 5. Nakumbuka kuhesabu, tangu moja hadi kenda, wakati ‘likuwa tabu, ikiwa inanishinda, chonde chonde taratibu, mlezi akanifunda, NI NANI KAMA MWALIMU, HUSUSAN WA MSINGI? 6. Leo miye mhasibu, taasisi ya takwimu, mdogo wangu tabibu, jijini Darisalamu, si kwa bahati nasibu, ni matunda ya mwalimu, NI NANI KAMA MWALIMU, HUSUSAN WA MSINGI? 7. Wanoitwa wata’lamu, wa’zo maridhawa fani, alowafunda mwalimu, leo wakuu nchini, mlezi wangu mwalimu, sana ninakuthamini, NI NANI KAMA MWALIMU, HUSUSAN WA MSINGI? 8. Kumbukeni ni mwalimu, wa mataifa mlezi, alowagea elimu, wa dunia welekezi, kiongozi ufahamu, yoyote uliyo ngazi, NI NANI KAMA MWALIMU, HUSUSAN WA MSINGI? 9. Na wasifa wake jama, haumaliziki wala, ndefu ja hadithi kama, alufu lela ulela, namuombea salama, nipulike wangu Mola, NI NANI KAMA MWALIMU, HUSUSAN WA MSINGI? 10. Subukhana shukurani, beti kumi kutimia, yaliyokuwa moyoni, hadhira nimepatia, na baraka maishani, walezi n’kiwatakia, NI NANI KAMA MWALIMU, HUSUSAN WA MSINGI? ********* Rwaka Kagarama, (Mshairi Mnyarwanda). Jimbo la Mashariki, Wilaya ya Nyagatare,RWANDA. |