SHAIRI: MASKINI WA BAHATI TAJIRI WA MIKOSI - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI: MASKINI WA BAHATI TAJIRI WA MIKOSI (/showthread.php?tid=1971) |
SHAIRI: MASKINI WA BAHATI TAJIRI WA MIKOSI - MwlMaeda - 01-03-2022 1. Jamani hii mikosi, kwangu inafata nini Kuniandama kwa kasi, kosa langu silioni Si mchana si weusi, na mimi hatuachani MASIKINI WA BAHATI, TAJIRI WA MIKOSI 2. Kila ninapodadisi, kisa chake sibaini Ni mimi mwenye nuksi, pekeyangu duniani kwa wenzangu haigusi, ni kwangu ndio nyumbani MASKINI WA BAHATI, TAJIRI WA MIKOSI 3. Bahati imenihasi, kwangu haionekani Inanipita kwa kasi, tukikutana njiani Mwenyewe ninajihisi, ninahitilafu fulani MASKINI WA BAHATI, TAJIRI WA MIKOSI 4. Ninamuomba kudusi, mwenye nguvu duniani Aniondolee nuksi, nami niwe furahani Anipe japo kiasi, riziki asinikini MASKINI WA BAHATI, TAJIRI WA MIKOSI 5. Kuhakikisha mikosi, ngoja niwachekesheni Hata ningepewa pasi, ya mpira kiwanjani Tagonga kwenye utosi, au upige puani MASKINI WA BAHATI, TAJIRI WA MIKOSI 6. Naililia bahati, ifike kwangu nyumbani Niipishe kwenye kiti, mwenyewe nikae chini Niipigie magoti, kuiomba samahani MASKINI WA BAHATI, TAJIRI WA MIKOSI 7. Kila nikijizatiti, mipango ya kila fani Ili ujao wakati, nami nile kivulini Hiyo raha siipati, inaishia ndotoni MASKINI WA BAHATI, TAJIRI WA MIKOSI 8. Nimekaa najihisi, chakula kipo mezani Njaa inanifilisi, chakula nakitamani Tatumbukia papasi, chakula nakitamani MASKINI WA BAHATI, TAJIRI WA MIKOSI 9. Usiku ninauhisi, najitupa kitandani Kwanza nitoe kamasi, niipate afueni Niikabidhi nafusi, kwa mola aloyakini MASKINI WA BAHATI, TAJIRI WA MIKOSI 10. Mafisi yano nigasi, ninashituka ndotoni Ninakimbia kwa kasi, kituo ni uwanjani Jamani hii mikosi, kwangu itaisha lini? MASKINI WA BAHATI, TAJIRI WA MIKOSI Mchapishaji Rajabu Salimu Abdul-razaq ?0659392247 Mtunzi ?ISMAIL RAJABU MPINI ? 09/04/1996 Mahali ?Kongwa-Magereza (Dodoma) >>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>> 1. Maisha uvumilivu, tafakuri kutumia, Usithubutu uvivu, juhudi kuzitegea, Huwezi kupata mbivu, ilhali wasinzia, PAMBANA YA HELA YOTE, UTATOBOA LAZIMA. 2. Uamkapo mapema, Riziki kujiwahia, Chagua yaliyo mema, Upate kujifanyia, Epuka kushika tama, Kombo yakikuendea, PAMBANA YA HELA YOTE, UTATOBOA LAZIMA. 3. Chagua kazi halali, Hutopata kashikashi, Utavuna nyingi mali, Bila wowote ubishi, Ishike yangu kauli, Uovu sikufundishi, PAMBANA YA HELA YOTE, UTATOBOA LAZIMA. 4. Kazi zote za haramu, Epuka hatua miya, Zidisha yako Nidhamu, Kipato kitatuliya, Sijifanye kichwa ngumu, Shauri kutopokeya, PAMBANA YA HELA YOTE, UTATOBOA LAZIMA. 5. Bini Rajabu Mpini, Tamaa sijejikatia, Katuleta duniani, Riziki mekadiria, Insi nao majini, Wote watajitwalia, PAMBANA YA HELA YOTE, UTATOBOA LAZIMA. 6. Kalamu imepasuka, Wino inajimwagia, Beti nilizoandika, Zakutosha fikiria, Nakwambia kukuruka, Riziki kujitwalia, PAMBANA YA HELA YOTE, UTATOBOA LAZIMA. Mtunzi: Moh’d Potea (Mikpot) Historia ilofifi Kilwa – Tanzania 31 – 03 – 2019 11:57 |