SHAIRI : CHUMBA CHA GIZA - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI : CHUMBA CHA GIZA (/showthread.php?tid=1954) |
SHAIRI : CHUMBA CHA GIZA - MwlMaeda - 01-03-2022 Wengi mmekusanyika, nduzangu na majirani Sauti zinasikika, zilo na tele huzuni Yanenwa nimeitika, wito wa Mola Manani Gogo mwataka lizika, mimi ni chumba cha giza Vilio mnavyolia, havinipi afuweni N’nazidi didimia, n’naona hamuoni Lau mnganisikia, mngazama ugangani Gogo msije lizika, mimi ni chumba cha giza Amenifanya ndondocha, izidi yake thamani Zinanirefuka kucha, hususa za mikononi Wallahi kila kukicha, mabadiliko mwilini Gogo msende lizika, mimi ni chumba cha giza Meno nayo yanyooka, yanaelekea chini Mdomoni yashatoka, sasa yapo kidevuni Ili niwe mkomboka, gogo lisende mavani Gogo msende lizika, mimi ni chumba cha giza Mama yangu hajiwezi, yuwalia kama nini Na ajala toka juzi, ale ana raha gani? Wasaidie Mwenyezi, ukweli waubaini Gogo wasende lizika, mimi ni chumba cha giza Ustadhi anenayo, kaegama kwenye dini Nami yaniumizayo, ni haya ya uchawini Hakika uchawi ndiyo, uloniweka chumbani Gogo msende lizika, mimi ni chumba cha giza Lau ndugu mtashika, ya mnyonge mnyongeni Yote alosema kaka, Makame yakubalini Huku ndipo ntatoka, n’tarudi duniani Gogo msende lizika, mimi ni chumba cha giza Nasikia m’mepanga, mkanizike nyumbani Kwenye mkoa wa Tanga, Moa kwetu kijijini Haya n’nashusha tanga, nenda kufa udongoni Gogo bure mtazika, mimi ni chumba cha giza Kwaheri ya kuonana, mkono wangu shavuni Haingalipo namna, ningalia ifaeni Moto hauwaki tena, umezimwa na jirani Gogo linaendazikwa, mimi ni chumba cha giza Mbaruku Ally Moto wenu Abtali Mjaala 03:12 usiku 19/05/2019 Nikiwa Kigogo Dsm Mzaliwa Moa Tanga |