FASIHI YA KISWAHILI NADHARIYA NA UHAKIKI: MUHADHARA WA SABA - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Chuo (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=3) +---- Forum: Shahada (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=20) +----- Forum: Nukuu (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=22) +----- Thread: FASIHI YA KISWAHILI NADHARIYA NA UHAKIKI: MUHADHARA WA SABA (/showthread.php?tid=1847) |
FASIHI YA KISWAHILI NADHARIYA NA UHAKIKI: MUHADHARA WA SABA - MwlMaeda - 12-27-2021 MUHADHARA WA SABA MAGHANI NA NGOMEZI
Maghani ni ushairi unaoghaniwa au kutambwa hadharani. Sauti ya mghani aghalabu huwa kati ya mazungumzo na kuimba (hazungumzi wala haimbi).Maghani hutambwa hadharani pamoja na ala za muziki au bila ala na huzungumzia masuala mazito ya kijamii au ya kibinafsi. Tanzu za maghani (i) Ghani nafsi; Ni ushairi simulizi wa kinafsi unaoelezea hisiya, matatizo na fikra za mtunzi mwenyewe. Mashairi ya mapenzi yanaingia katika kundi hili. (ii) Ghani tumbuizi; Ni ushairi wa kuliwaza, kufurahisha na kuburudisha na hughanwa badala ya kuimbwa. (iii) Ghani sifo; hili ni kundi mahususi la maghani ambalo hubeba tungo za kusifu hasa watu,wayama,mimea au vitu. Tanzu za ghani sifo (a) Vivugo/kivugo; ni ghani la kujisifu ambalo hutungwa na kughaniwa na mhusika mwenyewe. Muundo wake hutegemea sababu za mtunzi na jadi ya utunzi. Mathalan jamii ya wahaya kivugo huwa na mambo yafuatayo: – Jina halisi au jina la sifa ya mtunzi – Sifa za nasaba yake ya kuumeni – Sifa za nasaba ya kikeni – Maelezo ya matendo makuu aliyoyatenda au matendo matukufu yanayozidi wengine wote – Ahadi ya kutenda makubwa zaidi kwa ajili ya mkubwa wako – Tamati- kujikabidhi rasmi kwa mkubwa. (b) Tondozi; Ni tungo za kusifu watu, wanyama au vitu vya kawaida. Pembezi ni aina moja wapo ya tondozi ambayo husifu watu wakubwa au watawala. Tondozi zinazohusu wanadamu moja kwa moja ndio nyingi zaidi. Watu husifia wapenzi wao,adui zao au wake zao. Ghani simulizi; Ni ghani za kihadithi zenye mtiririko wenye msuko wa matukio uliojengwa ili kuleta taharuki na ujumbe fulani. Tanzu za ghani masimulizi ni: (a) Rara; Ni ghani zinazotambwa ili kusimulia hadithi, historia au tukio fulani na mara nyingi huambatana na muziki wa ala. Mtambaji huitwa Yeli/Manju na huwa ni mtaalamu wa kupiga ala fulani za muziki. Ala mashuhuri ni zeze, marimba, ngoma na njuga. Sifa za rara – Huweza kuwa tenzi au tendi – Lazima ziwe ni tungo za kishairi – Isirudie hadithi au tukio kwa kirefu – Matini yake hutungwa papo kwa papo (b) Tendi; huu ndio utanzu mashuhuri zaidi katika kundi la ghani simulizi, utendi ni utungo mrefu unaosimulia matukio ya kishujaa yenye uzito wa kijamii au matukio ya kitaifa. Huweza kuwa ya kihistoria au yaliyochanganya historia na visakale au visasili. Sifa za tendi – Muundo wa kinudhumu (kishairi) – Huwa na beti nyingi kati ya 700/800 – Upatanifu au muunganiko – Maudhui kuhusu maisha na matendo ya kishujaa. Ngomezi/ngoma;Ni fasihi ya ngoma ambapo baadhi ya makabila hupeleka habari kwa njia ya ngoma kupitia midundo fulani ambayo huwakilisha kauli fulani katika lugha ya kabila hilo. Utunzi wa ngoma hutumia kanuni na kaida za kimapokeo zinazofahamika kwa watu wengi katika jamii husika. Umbo la ujumbe wa ngoma huwa ni la kishairi. Matukio ya dharura kama vita, hutangazwa kwa njia ya ngoma. Sanaa ya ngoma haijachunguzwa kiasi cha kutosha na huenda ugunduzi huu ukapotea bila kuacha kumbukumbu za kuridhisha kama hazitachunguzwa kwa kina. |