MBINU ZA KUFUNDISHIA - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Chuo (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=3) +---- Forum: Stashahada/Cheti (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=21) +----- Forum: Nukuu (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=25) +----- Thread: MBINU ZA KUFUNDISHIA (/showthread.php?tid=168) |
MBINU ZA KUFUNDISHIA - MwlMaeda - 06-21-2021 MBINU ZA KUFUNDISHIA Mbinu za kufundishia, ni miongozo mbalimbali atumiayo mwalimu wakati wa kufundisha somo aliloliandaa kwa wanafunzi wake. Walimu wanapaswa kuamua kwa kuchagua kwa makini njia na mbinu bora za kufundishia ili wanafunzi wake waweze kujifunza kwa ufanisi. Ziko njia nyingi za kutengeneza mazingira ya mtoto aweze kujifunza na pia ziko mbinu nyingi za kufundishia. Pamoja na wingi huo tunaweza kuzigawa katika makundi makuu mawili kadri ya jinsi zinavyowashirikisha watoto katika tendo la kujifunza, ambazo tunaweza kuziita shirikishi na zisizo shirikishi.
Zifuatazo ni baadhi ya mbinu shirikishi na zisizo shirikishi za kufundishia pamoja na faida na hasara zake:-
Njia ya majadiliano, njia hii imekuwa ikitumika katika ufundishaji kwa muda mrefu. Katika kujadiliana mwanafunzi mmoja mmoja hupata nafasi ya mawazo aliyonayo kuhusu suala linalojadiliwa na yeye pia huweza kupata mawazo yaw engine. Katika majadiliano mwanafunzi hupata ujuzi mpya nje na ule aliokuwa nao kabla hajashiriki katika majadiliano.
Mambo ya kuzingatia.
Faida za mbinu.
Ø Kukuza mahusiano ya wahusika.
Ø Kuwafanya wahusika wafurahie na kulipenda somo.
Ø Kukuza stadi za ubunifu na mawasiliano.
Ø Kujenga uwezo wa wahusika wa kuamini na kuvumiliana.
Ø Huleta ujuzi na uongozi.
Ø Kila mmoja huweza kutoa mchango wake na mawazo yake kwani watu ni wachache katika kundi.
Ø Husaidia kujenga kumbukumbu kwa wanafunzi.
Hasara za mbinu hii.
Ø Kama hakuna usimamizi na utaratibu mzuri njia hii inaweza isiwe tofauti na mhadhara kwani mtu mmoja tu au kiongozi anaweza kutawala uwanja wa mazungumzo.
Ø Kama kiongozi si imara, kundi linaweza kushindwa kujadili mada waliopewa na hivyo kujadili nje ya mada.
Ø Hujenga uhasama kati ya kundi na kundi, wanafunzi na wanafunzi.
Njia ya mhadhara, hii ni njia ya kufundishia kitu kwa kutumia hotuba ndefu. Lengo la kutumia njia hii ni kuwazoeza wanafunzi kuwa wasikivu na kuzingatia mambo muhimu na yenye msingi tu kati ya maelezo mengi yanayotolewa na mhadhiri.
Mambo ya kuzingatia katika mbinu hii.
Faida za mbinu hii.
Ø Huwezesha kufundisha mambo mengi kwa wakati mmoja.
Ø Humjengea mwanafunzi tabia ya kuchambua taarifa na kuzingatia mambo muhimu tu.
Ø Inapima usikivu wa mwanafunzi kuhusu mada inayofundishwa.
Hasara za mbinu hii
Ø Haiwashirikishi sana wanafunzi katika tendo la kujifunza.
Ø Huwachosha wanafunzi kwa sababu watoto hawawezi kuwa wasikivu kwa muda mrefu.
Ø Wanafunzi huchoka kusikia sauti ya mtu mmoja tu muda wote.
Ø Ni mtu mmoja tu anayetoa mawazo yake na wengine yaani wanafunzi hupokea tu, hivyo hujenga utegemezi kwa wanafunzi.
Kazi mradi, wanafunzi na walimu wengi wameelekea kuamini kuwa mbinu ya kazi mradi ni ya utendaji wa mda mrefu. Kwa wengi kazi mradi inatumika tu kwa kuwatathimini wanafunzi kwa muda huo mrefu. Kwa mtazamo wa sasa kazi mradi yaweza kufanyika hata kwa kipindi kimoja tu cha darasani. Katika utendaji wanafunzi huunda maana zao binafsi kutokana na jinsi nadharia husika zinavyojitokeza katika maisha halisi ya kila siku.
Mambo ya kuzingatia katika mbinu hii.
Faida za mbinu hii.
Ø Kukuza stadi mbalimbali za kufikiri.
Ø Kujenga tabia ya kuhusisha mambo wanayojifunza na maisha yao ya kila siku.
Ø Kujiamini na kupenda kujifunza kwa kujitegemea.
Hasara ya mbinu hii.
Ø Ni vigumu kuchagua mada ifaayo kufundisha kwa njia hii.
Ø Kama haikuandaliwa vizuri maarifa au ujenzi wa maana uliokusudiwa hushindwa kuwafikia walengwa.
Njia ya ziara, hii ni safari inayopangwa kwa madhumuni fulani. Hii ni dhiara ya kielimu ambayo hufanywa kwa njia ya kutembelea na kuona mahali ua vitu halisi kwa njia ya kujifunza. Katika mazingira ya kishule waalimu hufanya ziara na wanafunzi wao kutembelea sehemu mbalimbali zenye mambo yanayohusiana na mada wanazofundisha shuleni. Wanafunzi wanaweza kutembelea sehemu kama vyanzo vya mito, madimbwi, viwanda, benki, posta na mbuga za wanyama.
Mambo ya kuzingatia katika mbinu hii.
Faida za mbinu hii.
Ø Humpa mwanafunzi nafasi ya kuwa katika mazingira halisi wakati wa kujifunza.
Ø Hufanya dhana dhahania kueleweka kwa kina zaidi.
Ø Huongeza motisha na kumuwezesha mwanafunzi kupenda kujifunza zaidi.
Ø Huondoa utata unaoweza kuwepo kutokana na mawazo ya awali ya wanafunzi na kuwafanya wajenge dhana kamilifu zaidi.
Ø Hushirikisha wanafunzi wote.
Ø Wanafunzi hutegemea katika kupata taarifa inayotakiwa badala ya kumtegemea mwalimu.
Hasara ya mbinu hii.
Ø Gharama huwa kubwa – usafiri.
Ø Matayarisho huchukua muda mrefu.
Ø Usimamizi huwa mgumu hasa kama darasa lina wanafunzi wengi na mahali pa ziara ni mbali.
Ø Sio rahisi kuendesha somo kwa kipindi kimoja tu.
Onyesho mbinu, ni uwasilishaji unaofanywa wa matendo kuhusu jambo au dhana fulani. Onesho mbinu huambatana na maelezo ya ana kwa ana, Matumizi ya zana na maswali na majibu ambayo huwezesha wanafunzi kujifunza stadi mpya.
Mambo ya kuzingatia katika mbinu hii.
Faida za mbinu hii.
Ø Kujifunza kwa kuona kuna mahamasisho makubwa katika kujifunza.
Ø Kujenga ari ya kujifunza.
Ø Wanafunzi hujifunza kwa kutenda chini ya kiongozi au mtaalamu.
Ø Njia hii huwezesha kufanya masahihisho ya moja kwa moja katika kujifunza.
Hasara za mbinu hii.
Ø Maandalizi makini hutakiwa na muda mwingi wa vitendo hutakiwa.
Ø Hairuhusu idadi kubwa ya wanafunzi.
Ø Maandalizi mabaya yanaweza kupotosha maana ya onesho.
Kwa kuhitimisha, inaweza kusemwa kuwa mbinu au njia za kufundishia na kujifunzia ni ujanja anoubuni mwalimu kila awapo darasani, kwa lengo la kurahisisha uelewekaji wa somo husika katika tendo la ufundishaji na ujifunzaji. Hivyo basi kila suala au jambo analolifanya mwalimu wakati wa somo darasani huweza kusemwa kuwa ni mbinu au njia ya kufundishia na kujifunzia.
MAREJELEO
Ø Mgombele J.Mwiga (2003). Mbinu za kufundishia na kujifunza: mwandiga bookshop.
Ø Jiandae.wordpress.com/zana za kufundishia.
Ø Paulmeela.wordpress.com/mbinu za kufundishia Kiswahili.
|