MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.

DHANA YA DIGLOSIA na TRIGLOSIA - Printable Version
JIFUNZE KISWAHILI
DHANA YA DIGLOSIA na TRIGLOSIA - Printable Version

+- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz)
+-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1)
+--- Forum: Sarufi na Utumizi wa lugha (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=9)
+--- Thread: DHANA YA DIGLOSIA na TRIGLOSIA (/showthread.php?tid=1606)

DHANA YA DIGLOSIA na TRIGLOSIA - MwlMaeda - 11-28-2021

DHANA YA DIGLOSIA na TRIGLOSIA
Dhana ya Diglosia
Dhana ya diglosia ilianzishwa na Ferguson mnamo mwaka wa 1959. Ferguson alianzisha dhana ya diglosia kutoka kwa neno la kifaransa Diglossie, Di ikimanisha mbili na glossie ikimanisha lugha. Kwa mujibu wa Sebba (2011), Ferguson alianzisha dhana hii kuelezea hali ya matumizi ya lugha ambapo lugha moja iliweza kutumiwa kwa njia mbili tofauti na wazungumzaji wake kukidhi mahitaji mbalimbali ya kijamii. Furaha (1991), anaongeza kuwa diglosia ni ile hali ya mzungumzaji kutumia namna moja ya lugha katika muktadha mmoja na namna nyingine ya lugha hiyo hiyo katika muktadha mwingine.
Kwa hivyo, kwa mujibu wa Hudson (1980), lugha moja inaweza kuwa na hadhi mbili tofauti kimatumizi kutegemea muktadha yaani hadhi ya juu na ya chini. Hadhi ya juu ya lugha ile ingetumika katika miktadha rasmi na hadhi ya chini ya lugha ile ile ingetumika katika miktadha isiyo rasmi katika jamii hiyo hiyo. Ferguson basi, kwa mujibu wa Furaha (1991), alielezea diglosia kama tukio ambalo lingewezekana tu katika mazingira ya lugha moja pekee. Hata hivyo Fishman, kama asemavyo Hudson (1980), mnamo mwaka wa 1971 alielezea uwezekano wa diglosia kujitokeza katika lugha mbili tofauti katika jamii moja. Katika mazingira kama haya, lugha moja huwa na hadhi ya juu na nyingine hadhi ya chini kimatumizi katika jamii ile (Furaha 1991).
Akielezea zaidi kuhusu diglosia, Sebba (2011) anasema kuwa Fishman alianzisha diglosia iliyo ama isiyo na uwililugha na uwililugha ulio ama usio na diglosia. Hivi, dhana ya diglosia inazua mazingira manne tofauti ya matumizi ya lugha yafuatayo:-
a) Mazingira ya kwanza ni ya uwililugha ukiwa na diglosia. Hapa lugha mbili katika jamii moja hutumika lakini zikiwa zimetenganishwa kabisa na majukumu zinayoyatekeleza. Lugha moja basi huwa na hadhi ya juu kimatumizi kuliko ile nyingine
b) Pili, kuna mazingira ya uwililugha bila diglosia na ambayo ni nadra sana kupatikana katika jamii, ambapo lugha mbili hutumika katika jamii lakini hakuna ile iliyo na hadhi kuliko nyingine
c) Katika mazingira ya tatu, Sebba anasema kuwa hapa kuna diglosia bila uwililugha ambapo lugha moja tu ndiyo inayotumika katika jamii lakini hupewa hadhi tofauti katika miktadha tofauti.
d) Mwisho, kulingana na Sebba, ni mazingira ambamo hamna diglosia ama uwililugha. Hii ina maana kuwa ni lugha moja inayotumika katika jamii bila hadhi zozote kujitokeza katika miktadha tofauti.
Mataifa mengi ya Kiafrika yana mifumo ya uwililugha na diglosia ambapo lugha mbalimbali zinazotumika hapa hupewa hadhi tofauti kimatumizi (Hudson 1980, Sebba 2011). Lugha za kikoloni kama vile Kiingereza, Kifaransa na Kijerumani huwa zimepewa hadhi ya juu kimatumizi ikilinganishwa na lugha za mama ambazo hupewa hadhi ya chini kimatumizi.
Dhana ya Triglosia
Mkilifi (1972) alizua dhana ya triglosia alipokuwa akitafiti kuhusu matumizi ya lugha nchini Tanzania. Hapa alilinganisha lugha ya Kiingereza, Kiswahili na lugha za mama kimatumizi. Lugha ya Kiingereza ilikuwa na hadhi ya juu ikilinganishwa na Kiswahili. Hata hivyo, lugha ya Kiswahili ilikuwa na hadhi ya juu ikilinganishwa na lugha za mama kimatumizi katika jamii zile zile.
Batibo (2005) anaeleza kuwa mataifa mengi ya Kiafrika yana mpangilio wa triglosia katika matumizi yake. Lugha za kikoloni (Kiingereza, Kifaransa, Kireno n.k) huwa na hadhi ya juu na hutekeleza majukumu rasmi kama vile shughuli za kielimu na kiserikali. Chini ya lugha hizi ni zile za kiasili za matumizi mapana kama vile Kiswahili na ambazo hutumika katika masuala ya kijamii na kiuchumi. Chini kabisa huwa lugha za mama ambazo huwa na hadhi ya chini kabisa na huachiwa majukumu yasio rasmi wala muhimu katika jamii. Hadhi za juu na hadhi za chini za lugha ndizo huzua mielekeo ya lugha miongoni mwa wazungumzaji kwani lugha nyingine hupendelewa zaidi kuliko nyingine kimatumizi.
Suala la diglosia na triglosia lilikuwa muhimu kwa utafiti wetu kwani liliwezesha mtafiti kuelewa bayana mpangilio ya lugha kihadhi hasa katika jamii zilizo na hali ya wingilugha. Eneo la utafiti wetu lilkuwa katika miji ya Nairobi, Kiambu na Thika ambako tulichunguza matumizi ya lugha za Kikuyu, Kiswahili, Kiingereza na Sheng miongoni mwa vijana wa jamii ya Kikuyu. Mipangilio ya lugha ama kidiglosia au kitriglosia katika jamii ndio huzua suala la mielekeo ya lugha. Utafiti huu ulilenga kubaini mielekeo walio nayo vijana wa jamii ya Kikuyu mijini Nairobi, Kiambu na Thika kuhusu lugha ya Kikuyu ikilinganishwa na lugha za Kiswahili, Kiingereza na Sheng. Kama ilivyobainika katika matokeo ya utafiti huu, vijana wa jamii ya Kikuyu katika miji ya Nairobi, Kiambu na Thika wana mielekeo chanya kuhusu lugha za Kiswahili, Kiingereza na Sheng ikilinganishwa na mielekeo hasi waliyo nayo kuhusu lugha ya Kikuyu. Utafiti huu pia ulibaini kuwa mielekeo hasi ya vijana wa jamii ya Kikuyu mijini Nairobi, Kiambu na Thika ndiyo huathiri umilisi wao wa lugha za mama kama vile lugha ya Kikuyu jambo ambalo nalo hatimaye kuathiri uthabiti wa kiisimujamii wa lugha ya Kikuyu mijini.