MIIKO YA WASWAHILI/WAAFRIKA NA TAMADUNI ZA ULIMWENGU - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Historia ya makabila ya kibantu (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=15) +--- Thread: MIIKO YA WASWAHILI/WAAFRIKA NA TAMADUNI ZA ULIMWENGU (/showthread.php?tid=16) |
MIIKO YA WASWAHILI/WAAFRIKA NA TAMADUNI ZA ULIMWENGU - MwlMaeda - 06-14-2021 MIIKO YA WASWAHILI/WAAFRIKA NA TAMADUNI ZA ULIMWENGU
Pamoja na mambo mengine mengi, mgeni au wageni hupenda kujifunza tamaduni za wenyeji. Hata kama watazidharau lakini lazima kwanza wazijue. Mimi na wewe tunaweza kuwa wageni ndani au nje ya nchi. Moja ya mambo ambayo tungejifunza ugenini ni utamaduni wa wenyeji wetu.
Au mimi na wewe tunaweza kuwa wenyeji, moja ya mambo ambayo wageni wetu wangependa kujifunza kwetu ni utamaduni wetu. Kwa ainisho la ujumla, utamaduni ni dhana inayokusanya mila, miiko, adabu, desturi, lugha, vyakula na kadhalika.
Kila jamii ina utamaduni wake. Waafrika na hasa Watanzania tuna miiko yetu ya kiutamaduni ambayo tungependa wageni waiheshimu. Baada ya kipindi cha kutawaliwa kikoloni, sasa tuna uhuru wa kulinda utamaduni wetu.
Yawezekana, kwa kiasi fulani, uhuru huu wa kulinda utamaduni wetu unatatizwa na umasikini wetu unaotulazimu kuomba misaada kwa wahisani lakini bado uungwana wetu hauuawi na umasikini.
Yawezekana Mtumwa akakosa hiyari kwa sababu ya maisha ya utumwani. Lakini masikini ana nafasi ya hiyari licha ya umasikini wake. Jamii yetu ina mila zake, na Taifa letu ni masikini, bado mila zetu haziwezi kuuawa kwa sababu ya umasikini wetu.
Tena eneo la utamaduni nalo pia sasa linaweza kuwa moja ya vivutio vya utalii. Watalii wanataka kuja kuona na kujifunza utamaduni wetu halisi. Wanawapenda Wamasai kwa sababu ya kubaki katika utamaduni wao halisi. Hatusemi kuwa kila cha utamaduni wetu kifuatwe au kisiachwe hata kama ni kibaya.
La hasha! Kile ambacho hakifai lazima kiachwe. Kama utamaduni unazuia watoto kusoma na wabaki kuchunga ng’ombe, hiyo hapana! Utamaduni huo uachwe mara moja. Si utamaduni bali ni ujinga huo.
Kama utamaduni unakeketa viungo vya uzazi, haufai kabisa! Uachwe mara moja au utungiwe sheria ya kuukomesha! Tungependa wageni wetu wajifunze mazuri ya utamaduni wetu, na tusingependa wajifunze mabaya ya utamaduni wetu.
Mazuri yako mengi mno, kuanzia Lugha yetu ya Kiswahili, mavazi yetu, vyakula vyetu, ushujaa wetu, maungwana yetu, ukarimu wetu, heshima yetu kwa wazazi, heshima yetu kwa wakwe zetu, adabu za mke kwa mume, na mume kwa mke na kadhalika.
Haya ni mambo mazuri kabisa. Tusijidharau katika haya hata kidogo, na tuwe ngangari katika kuyaenzi yote hayo. Lugha yetu ya Kiswahili ina nafasi kubwa katika utamaduni wa Lugha ulimwenguni.
Utamaduni wetu wa lugha una nafasi ya kupata heshima kubwa na kututambulisha popote pale. Kuitwa Mswahili kwaweza kuwa fahari ya kilimwengu. Lakini hii itategemea msimamo wetu katika kuuenzi utamaduni huu.
Nitaje maeneo kadhaa ambayo labda bado yanaonesha udhaifu wetu wa kutojiamini pale linapokuja suala la lugha yetu. Mosi, tunapotembelewa na wageni ambao wao wenyewe hawatumii Lugha ya Kiingereza, ingelikuwa fursa nzuri na sisi kutumia Lugha yetu.
Kama mgeni wa Kichina au Kijerumani anakuja nchini na kutumia lugha yake, kwa nini wenyeji wake tutumie lugha nyingine ya kigeni kuwasiliana naye?
Mjerumani au Mchina anapokwenda Uingereza au Marekani, anatumia Kijerumani au Kichina chake huku mwenyeji wake akitumia Kiingereza chake. Inakuwaje Mjerumani na Mchina huyo huyo anapokuja Tanzania, mwenyeji wake anatumia Lugha ya Waingereza kuwasiliana naye.
Ni lini Afrika itajikomboa na utumwa wa Kilugha? Mjerumani ambaye alitutawala anajua sana Watanzania tunayo lugha yetu ya Kiswahili, na kwa kuheshimu nafasi ya Kiswahili ulimwenguni, Ujerumani ina Shirika kubwa la Habari linaloendesha matangazo yake kwa Lugha ya Kiswahili.
Isitoshe, kuna Wajerumani kadhaa wanaozungumza au kujifunza Kiswahili. Ni dhahiri mgeni wa kidiplomasia wa Ujerumani angetarajia kukutana na Kiswahili katika mawasiliano na mwenyeji wake.
Yawezekana kuna tatizo la ukalimani lakini kwa nini? Miaka mingi ya uhuru ingeliweza kabisa kutupatia wakalimani wa angalau lugha zote kubwa za Ulimwengu kikiwemo Kijerumani.
Kwa kuwa Mjerumani hakuja kwenye Kiingereza basi na sisi tusingekuja katika lugha hiyo. Tungebaki na yetu, na bila shaka na yeye angetuelewa. Hata kama tunabanwa na ukweli kuwa sisi ndio wahitaji, na wenzetu ndio wahisani, lakini kwa kuwa muhisani huyu ana lugha yake, lugha yetu nayo ingekuwa na nafasi.
Kama angelikuwa Obama au Cameron, hapo tungebaki na Lugha yao ambayo kwetu pia ni lugha rasmi ya mawasiliano. Hatuna tatizo na Kiingereza, na wala viongozi wetu hawafanyi kosa lolote kukitumia, lazima tukubali nayo pia ni lugha yetu kuu ya kufundishia sekondari na vyuoni, hatuna namna ya kukwepa.
Lakini katika kujaribu kukipandisha hadhi ya Kimataifa Kiswahili, ipo mianya ambayo tunaweza kuitumia kupenyeza Kiswahili iwe katika dhifa za kidiplomasia au penginepo. Hasa pale tunapofikiwa na wageni wasiotumia Kiingereza.
Siku alipokuja Rais wa Ujerumani, waandishi wetu wengi wenye udhaifu mkubwa wa Lugha ya Kiingereza wangeweza kutumia Kiswahili chao kuuliza maswali, na kisha Mkalimani wa Kijerumani kutafsiri.
Lakini ule utambulisho tu wa Ikulu ulitosha kuwanyamazisha wale wasioujua Kiingereza. Kwamba ni umombo uliohitajika! Wasiokimanya Kiingereza wakabaki na maswali yao huku wakiwakilishwa na watu ambao maswali yao hayakulenga maeneo ambayo wengi wangeyatarajia.
Tunajifunza kutokana na makosa, na kwa hili si kwamba tunalaumiana lakini tuyasome upya mazingira ya kidiplomasia na kuona wapi tunaweza kubaki Waswahili kilugha, na wapi tunalazimika kutumia Kiingereza.
Pili, tuna miiko yetu ya Kimaadili katika eneo hilohilo la utamaduni. Mswahili ana miiko ambayo, pengine, Mzungu hana. Na Mataifa yamekubaliana kuheshimiana kwa tamaduni zao.
Hivyo, mgongano wa utamaduni angalau unaweza kupunguzwa kama si kuepukwa. Viongozi wa Kimataifa huwa na kawaida ya kupiga picha za pamoja. Lakini upigaji picha nao wakati mwingine huzingatia utamaduni.
Kwa utamaduni wetu wa Waswahili, kupiga picha na mke au mume wa mtu ni mtihani kidogo! Japo inatokea hata Kitaifa lakini pale ambapo mume wa mtu yupo, na mke wa mtu yupo, ni vema picha ikazingatia hisia za unyumba wao.
Tusifiche, na sidhani kama nitamuudhi yoyote kwamba, Mama yetu alibabaika kidogo Siku tulipotembelewa na mgeni wa Ujerumani. Alikuwa nyuma ya baba, na mwenziwe naye alikuwa nyuma ya baba mgeni.
Mwenzio hakuwa na tatizo kwa sababu kwao wao mume kupiga picha na mke wa mwenziwe si tatizo. Tatizo likawa kwetu. Ulikuwa ni mgongano wa hadharani wa kiutamaduni. Baba alipogeuka nyuma akaona, mama wa Kizungu kishasogea.
Baba hakuwa na namna ila kumwita mama wa Kizungu. Mamaetu akapata majibu ya haraka aende wapi. Picha ikapigwa kwa utamaduni wa Kizungu, si utamaduni wetu wa Kiswahili. Bila shaka hii nayo ni changamoto.
Inaweza kutafutiwa njia mbili; ya kwanza Ikulu yetu ianze kutangaza utamaduni wetu wa kupiga picha kwa kuzingatia hisia za unyumba. Kila mtu asimame na mkewe. Au pili, waume wapige yao, na wake wapige yao. Sijui nje huko tutafanyaje lakini hapa ndani tujitahidi kuzingatia utamaduni wetu. |