TAASISI YA TAALUMA ZA KISWAHILI (TATAKI) - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Taasisi za kukuza lugha (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=18) +--- Thread: TAASISI YA TAALUMA ZA KISWAHILI (TATAKI) (/showthread.php?tid=1188) |
TAASISI YA TAALUMA ZA KISWAHILI (TATAKI) - MwlMaeda - 09-08-2021 Taasisi ya Taaluma za Kiswahili
Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) ni idara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania. Taasisi hii ni miongoni mwa taasisi kongwe za lugha nchini Tanzania. Madhumuni yake yakiwa ni kusimamia usanifishaji na maendeleo ya lugha ya Kiswahili. Hadi mnamo mwaka 2009 taasisi hii ilijulikana zaidi kwa jina la TUKI au “Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili“
Historia yake
Ilianzishwa mnamo mwaka 1930 kama Inter-territorial Language (Swahili) committee ya Nchi za Afrika ya Mashariki, baadaye ikaitwa Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki. Mnamo mwaka 1964 kamati ilifanywa kuwa Sehemu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaamu. Baadaye ikaitwa Chuo cha Uchunguzi wa Lugha ya Kiswahili. Tangu 1970 kimepewa jina la Taasisi ya Uchunguzi wa Lugha ya Kiswahili. Mwaka 2009, TUKI iliungana na iliyokuwa Idara ya Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuunda Taasisi kubwa zaidi inayoitwa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili – TATAKI
Majukumu
Mwanzoni, Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili ni taasisi ya utafiti ilipewa jukumu la kutafiti nyanja zote za lugha ya Kiswahili, fasihi na utamaduni, na kuchapisha matokeo ya utafiti huo. Hivyo pamoja na BAKITA (Baraza la Kiswahili Tanzania) TUKI ndiye mlinzi wa usanifu wa lugha ya Kiswahili katika Tanzania. Baada ya kuungana na Idara ya Kiswahili, sasa TATAKI inafundisha Isimu, Fasihi na Historia ya Lugha ya Kiswahili katika Shahada za Awali, Mahiri na Uzamivu.
Kazi yake
Kutafiti na kuchapisha matokeo ya utafiti katika nyanja mbalimbali za Lugha, Isimu na Fasihi ya Kiswahili, TATAKI inasimamia Tafsiri na Ukalimani. Inafundisha Kiswahili kama lugha ya pili hasa kwa wageni kutoka nje ya ulimwengu wa Waswahili na kuendeleza utungaji wa Kamusi mbalimbali zinazohusiana na Kiswahili. Kati ya kamusi hizi ni
TUKI imehariri toleo la Kiswahili la “Historia Kuu ya Afrika” iliyotungwa na kamati ya wataalamu ya UNESCO.
Taasisi ya Taaluma za Kiswahili ( TATAKI) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni asasi kongwe inayojishughulisha na ufundishaji, utafiti na utoajiushauri wa kitaaluma katika maendeleo ya lugha ya Kiswahili. TATAKI inadhamana ya kufundisha na kutafiti vipengele vyote vya lugha, kwa kuzigatia vipaumbele vya Chuo Kikuu cha Dar es salaam na Jamhuri ya muungano wa Tanzania. HISTORIA YA TATAKI TATAKI ni Taasisi yenye historia ndefu kuliko Taasisi zote zinazohusika na ukuzaji na uendelezaji wa lugha ya Kiswahili duniani. Historia ya TATAKI inaanzia mwaka 1930 ilipoanzishwa kamati ya lugha (ya Kiswahili) ya Afrika Mashariki. Mnamo mwaka 1961 Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilianzishwa kama Chuo Kikuu Kishiriki cha London. Kuanzia mwaka 1962, viongozi wa kamati waliaza kufikiria kuhamisha shughuli za kamati kwenye Chuo Kikuu kimojawapo. Vyuo vilivyofikiriwa ni Makerere na Dar es Salaam. Mwaka 1963 shughuli za kamati zilihamishiwa katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es Salaam na hatimye kamati ilibadili jina na kuwa Chuo cha Uchunguzi wa Kiswahili. Majukumu ya Chuo cha Uchunguzi wa Kiswahili hayakutofautiana na yale ya kamati ya lugha. Mwaka 1970 baada ya kuanzishwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ndipo Taasisi ya uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) ikaanzishwa chini ya ibara ya 22(3) ya sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Katika kipindi hiki ilianzishwa pia idara ya Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam iliyokuwa chini ya Kitivo cha Sanaa na Sayansi za Jamii. Miongoni mwa majukumu ya idara ilikuwa ni kufundisha lugha ya Kiswahili kwa wanafunzi kutoka ndani na nje ya Tanzania. Kuanzia mwanzoni mwa miaka 2000, Chuo Kikuu kilianza kupitia upya muundo wake ili kufanyakazi kwa ufanisi na weledi. Katika mchakato huo yalitolewa mapendekezo mbalimbali ilikiwa ni pamoja na kuunganisha vitengo ambavyo majukumu yake yalionekana kufanana. Kwa kuwa malengo ya idara ya Kiswahili na TUKI yalilenga kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili, mnamo mwaka 2009 iliyokuwa idara ya Kiswahili ikaungana na TUKI na kuunda Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI). Majukumu ya TATAKI sasa yamejikita katika utafiti wa Nyanja mbalimbali zihusuzo lugha na fasihi ya Kiswahili katika ngazi mbalimbali.
TATAKI inaidara mbili ambazo ni idara ya lugha ya Kiswahili na isimu na idara ya fasihi, mawasiliano na uchapaji. Idara hizi kwa pamoja zinashirikiana katika ufundishaji wa programu mbalimbali taasisini kama inavyoainishwa hapa chini:
PROGRAMU ZINAZOFUNDISHWA NA TATAKI
1. B.A. Kiswahili Ni shahada ya awali ambayo hutolewa katika muda wa miaka mitatu. Katika shahada hii, kozi mbalimbali za Isimu na Fasihi hutolewa. Masharti ya jumla ya udahili ya Chuo Kikuu huzingatiwa. Hata hivyo ili mwombaji adahiliwe katika programu ya B.A (kiswahili) anapaswa, pamoja na masomo mengine, awe amesoma somo la Kiswahili kidato cha tano na sita na kufaulu kwa wastani wa angalau alama D au awe na sifa zinazofanana na hizo. 2. M.A. Kiswahili Hii ni shahada ua umahiri ambayo hutolewa kwa Tamrini na Tasnifu katika Isimu na Fasihi kwa muda wa miezi 18 (Tamrini na Tasnifu); na miezi 24 (kwa Tasnifu pekee). Ili kujiunga na programu hii mbali na sifa za jumla za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwombaji anapaswa kuwa amefaulu masomo ya Kiswahili katika shahada za awali kwa WAKIA (GPA) isiyopungua 3.0 kwa kozi za Kiswahili. 3.PhD. Kiswahili
Masomo katika programu hii hutolewa kwa namna mbili. PhD kwa Tamrini na Tasnifu.PhD kwa Tamrini hutolewa kwa muda wa miaka minne na PhD kwa Tasnifu hutolewa kwa muda wa miaka mitatu. Ilikudahiliwa katika programu hizi mwombaji anapaswa kuwa amesoma Kiswahili au masomo yanayoendana na umahiri. Lugha inayotumika kufundishia na kuandika ripoti ya utafiti kwa programu zote ni Kiswahili. VITUO VYA TATAKI
Mbali na idara za ufundishaji, TATAKI pia hufanya kazi za kiutafiti kupitia vituo vya utafiti na ushauri. KITUO CHA FASIHI YA KISWAHILI NA MAPOKEO YA SIMULIZI YA KIAFRIKA
Miongoni mwa majukumu ya kituo hiki ni kuratibu na kusimamia shughuli zote za utafiti katika nyanja mbalimbali; kuandaa na kuchapisha Makala na vitabu vyo kufundishia kozi za fasihi, mawasiliano na uchapishaji kwa Kiswahili; kutafiti kuhusu kazi za wanafasihi mbalimbali wa zamani na sasa; kukusanya na kuhifadhi data, nyaraka na taarifu muhimuza kifasihi. KITUO CHA ISTILAHI, TAFSIRI, UKALIMANI NA TEKNOLOJIA YA LUGHA
Jukumu kuu la kituo hiki ni kutoa huduma zinazohusu masuala ya istilahi, tafsiri, ukalimani na teknolojia ya lugha. Kwa kiasi kikubwa kituo hiki hujihusisha na shughuli za tafsiri ya nyaraka mbalimbali kutoka katika asasi za kiserikali na zisizo za kiserikali. KITUO CHA KISWAHILI KWA WAGENI
Kituo hiki kinahusika na kuratibu shughuli zote za ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni. Wageni hufundishwa kwa vikundi au mtu mojamoja. Kituo pia kina mpango wa kujiimarisha na kuwa kituo cha weledi wa Kiswahili Ulimwenguni. KITUO CHA KAMUSI NA SARUFI YA KISWAHILI
Hujishughuliasha na kufanya utafiti wa msamiati mpya unaotumika katika jamii na kuukusanya kwa ajili ya kuboresha kamusi na vitabu vingine vya sarufi ya Kiswahili. Hivi sasa kituo kimeshatoa kamusi ya Kiingereza-Kiswahili na Kiswahili-Kiingereza kwa njia ya nakala ngumu na kwa njia ya simu ya kiganjani. Aidha kituo kwa kushirikiana na shirika la uchapishaji la OXFORD tawi la Nairobi wametoa matoleo kadhaa ya Kamusi ya Kiswahili Sanifu. UDAHILI WA WANAFUNZI
Wanafunzi wenye lengo la kusoma programu zinazotolewa na TATAKI hudahiliwa kwa kuzingatia taratibu zote za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. TAARIFA NYINGINE
TATAKI pamoja na kujishughulisha na ufundishaji, utafiti na utoaji ushauri, hujishughulisha pia na shughuli za uchpaji na uchapishaji. Uchapishaji hulenga kazi zilizoandikwa kwa lugha ya Kiswahili na uchapaji hufanywa kwa kazi zote bila kujali zimeandikwa kwa lugha gani ilimradi kazi hizo zizingatiye maadili ya uchapaji wa kitaaluma kama ilivyoinishwa katika Sera ya Uchapaji na Uchapishaji wa TATAKI. Aidha, TATAKI hutoa huduma ya ushauri wa kitaalamu kwa watu mbalimbali wakiwemo wanafunzi wa shule za sekondari na vyuo vya ualimu wanaokuja kufanyakazi mradi kwa lengo la kikamilisha matakwa ya kitaaluma katika masomo yao.
RE: TAASISI YA TAALUMA ZA KISWAHILI (TATAKI) - Faustin yahaya - 07-28-2022 Imekaa vizuri kaka |