TOFAUTI KATI YA SARUFI MIUNDO VIRAI NA SARUFI GEUZI - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Chuo (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=3) +---- Forum: Shahada (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=20) +----- Forum: Maswali na majibu (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=24) +----- Thread: TOFAUTI KATI YA SARUFI MIUNDO VIRAI NA SARUFI GEUZI (/showthread.php?tid=1088) |
TOFAUTI KATI YA SARUFI MIUNDO VIRAI NA SARUFI GEUZI - MwlMaeda - 08-31-2021 Tofauti kati ya Sarufi miundo virai na Sarufi geuzi
SWALI: Sarufi miundo virai inatofautianaje na Sarufi geuzi?
Sarufi ni nini ? Kihore na wenzake (2008) wakimnukuu Gaynor (1968:88) wanaeleza kuwa sarufi ni sayansi ya muundo wa lugha pamoja na sheria, kanuni na matumizi yake ambayo kwa kawaida hukubalika kwa watumiaji wake. Massamba na wenzake (2009:31) wanaeleza kuwa sarufi ni kanuni, sheria au taratibu za uchambuzi zinazotawala lugha. Saluhaya (2010:72) anadai kuwa sarufi ni kanuni, sheria au taratibu zinazotawala lugha katika matumizi yake ambayo hujumuisha matamshi, maumbo, miundo na maana. Taaluma hii husisitiza kanuni zitumikazo katika uchambuzi wa lugha katika viwango vinne vilivyotajwa hapo juu. Sarufi miundo virai Hiki ni kitengo cha sarufi geuza maumbo zalishi ambacho hujikita katika matumizi ya sheria chache kuzalisha sentensi nyingi zisizo na kikomo ambazo zina usarufi na hata zile ambazo hazijawahi kutungwa(Matinde, 2012:233). Sarufi miundo virai ni mkabala wa kuchambua lugha kwa kuigawa sentensi katika virai vinavyoiunda na kasha kuvichanganua zaidi hadi kufikia neon moja moja lililokiunda kirai. Sarufi Geuzi Sarufi geuzi ni utaratibu wa kubadili maumbo ya maneno kuwa maumbo mengine kwa kufuata kanuni maalumu. Sarufi hii hujengwa kwa wazo kwamba katika lugha kuna sentensi ambazo huwa ni za msingi, ambazo kutokana na kaida mahususi sentensi zingine huweza kuzalishwa na sentensi hizo (Matinde, 2012:231). Ugeuzaji huu huathiri muundo wa sentensi na wala si maana ya sentensi. Kwa mfano; (a) John amemchapa Bigile. (b) Bigile amechapwa na John. Hivyo basi, ugeuzaji ni mbinu ya kisarufi ambayo hutumiwa katika sarufi geuza maumbo zalishi kuzalisha sentensi lukuki kwa kufuta sheria au kanuni maalumu. Kwa mujibu wa Habwe na Karanja (2007), Matinde, (2012) wanaonesha utofauti uliopo kati ya sarufi miundo virai na sarufi geuzi kama ifuatavyo: Tofauti katika maana, sarufi geuzi maumbo ni utaratibu wa kubadili maumbo kuwa maumbo mengine kwa kufuata kanuni maalumu. Ilhali sarufi miundo virai ni kitengo cha sarufi geuzi maumbo zalishi ambacho hujikita katika matumizi ya sheria chache kuzalisha sentensi nyingi zisizo na ukomo. Tofauti katika uchanganuzi wa sentensi, sarufi geuzi huweza kuchanganua sentensi zenye maumbo tofauti. Kwa mfano sentensi sahili, changamano au ambatano ilhali sarufi miundo virai hujikita katika kuchanganua sentensi sahili peke yake. Mfano; Rajabu ni mwana wangu. Tofauti katika uchopekaji wa viambajengo, sarufi geuzi huweza kuchopeka viambajengo katika sentensi na kuifanya sentensi hiyo kuwa tenda au tendwa. Kwa mfano, sentensi ya kauli ya kutenda inapogeuzwa na kuwa katika hali ya kutendwa kuna elementi ambazo huchopekwa. Mfano; (a) Changwe anampiga mtoto (b) Mtoto anapigwa na Alpha. Hapa tunaona mofu {-w} na kihusishi {na} huchopekwa katika sentensi (a) na kuifanya sentensi hiyo kuwa ya kauli ya kutendwa katika (b). Ilhali sarufi miundo virai uchopekaji huo haujitokezi na hivyo kutokuonyesha mahusiano kati ya kauli tendi na tendwa. Tofauti ya waasisi, sarufi geuzi iliasisiwa na mwanasarufi aitwaye Noam Chomsky (1957) ambaye anadai kuwa nadharia hii ya sarufi geuzi ilizuka ili kurekebisha taratibu za sarufi za awali. Yeye alidai kuwa sarufi za awali hazingeweza kuonyesha kuwa sentensi ya kauli ya kutenda na ile ya kauli ya kutendwa zinatokana na muundo mmoja wa ndani. Pia sarufi za awali hazingeweza kuonyesha mahusiano ya sentensi zinazotofautiana kwa ndani lakini ambazo zilikuwa na muundo wan je mmoja. Kwa mfano; Herman alinunuliwa shati na mwanawe. Sura hii ya nje ya sentensi huwa ina sentensi kadhaa katika muundo wake wa ndani. Wakati sarufi miundo virai iliasisiwa na Bussmann (1996) ambaye anafafanua kwamba sheria miundo virai ni sheria zinazoonyesha mpangilio na ujenzi wa virai katika lugha, hivyo sheria hii huonyesha kuandikwa tena kwa viambajengo. Sheria kama, S = KN+KT yaani S = sentensi KN = kikundi nomino/kirai nomino KT = kikundi tenzi/kirai kitenzi Inamaanisha kuwa sentensi inaweza kuandikwa kama Kikundi Nomino kikifuatwa na Kikundi Tenzi. Wakati mwingine sheria miundo virai huonyesha uhusiano wa utawazi hivi kwamba nomino hutawala Kikundi Nomino (KN). Kwa mfano sentensi kama; Amina ni mke wangu. Suala la msingi ambalo wanaumuundo walisisitiza ni kutazama na kuchunguza lugha kisayansi. Hapa walisema kuwa masuala ilibidi yachunguzwe kwa uwazi na kuonyesha vitu, kategoria na elementi kwa uwazi zaidi. Ilhali sarufi geuzi hueleza ujuzi wa lugha ambao msemaji mzawa anao unaomwezesha kutumia lugha. Huu ni ujuzi wa kutunga sentensi kwa njia iliyo sahihi na vilevile namna sahihi ya kutamka na kueleza maana za maneno na sentensi. Mfano mmilisi wa lugha ya Kizinza anaweza kutunga sentensi zinazoeleweka na kutamka maneno ya lugha hiyo kwa usahihi kabisa. Kwa ujumla, sarufi miundo virai na sarufi geuzi hufanana sana katika kuchunguza miundo ya lugha husika japo katika utendaji wake hujitokeza baadhi ya tofauti ambazo husababisha nadharia hizi za sarufi miundo kutofautiana katika vipengele kadha wa kadha kama vile uchopekaji wa viambajengo, maana zake pamoja na mfumo wa namna ya kuchanganua sentensi. MAREJELEO Habwe, J. & Karanja, P. (2004). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili.Nairobi: Phoenix Publishers. Habwe, J. & Karanja, P. (2007). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili.Nairobi: Phoenix Publishers. Kihore, Y.M. na wenzake. (2008). Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu (SAMAKISA). Sekondari na Vyuo. Dar es Salaam: TUKI. Massamba, D.P.B na Wenzake (1999). Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu (SAMIKISA); Sekondari na Vyuo. Dar es Saalam: TUKI. Matinde, R.S. (2012). Dafina ya Lugha, Isimu na Nadharia; Kwa Sekondari, Vyuo vya Kati na Vyuo Vikuu. Mwanza: Serengeti Educational Publishers (T) LTD. Saluhaya, M.C. (2010). Nadharia ya Lugha Kidato cha Tano na Sita. Dar es Salaam: CHILDREN EDUCATION SOCIETY (CHESO). |